
DEREKHI AFRIKA
Dini ya Kiyahudi, Utamaduni wa Kiafrika
DEREKHI AFRIKA ni dhehebu jipya la Kikiristo ambalo linaanzishwa kuwaunganisha wakiristo wote milioni 700 katika nchi zote 42 za Afrika Kusini mwa Sahara, katika dhehebu moja, bila kujumuisha Ethiopia na Eritrea. Dhehebu hili, kwa hiyo, lina lengo la kuuchukua Ukiristo wote wa Afrika, na kuuendesha kitaasisi. Hatua hii ni Ufunuo wa Roho, na inaleta mabadiliko makubwa sana katika Ukiristo wa sasa.
1) KUTOKA UKIRISTO HADI UDEREKHI
Dini inayoitwa Ukiristo ulianzia pale Yerusalemu, mara baada ya Bwana Yesu kupaa mbinguni, ukiwa ni dini ya Wayahudi iliyoyakaribisha mataifa mengine yote. Ingawaje neno la Mungu linasema kila yeyote anayeamini ni Myahudi kwa imani, na ni uzao wa Ibrahimu (Gal 3:7), bado Wayahudi wa damu, Watoto wa Yakobo, wanabaki kuwa wenyeji wa dini hii, na sisi sote, Waafrika na Wazungu, ni ‘watu wa mataifa’ na tunaichukua dini kutokea kwao. Miaka michache baada ya dini hii kuanza hapo Yerusalemu, ilipewa jina la DEREKHI (Kiebrania cha NJIA). na iliendelea kuitwa hivyo kwa miaka 100. Neno Ukiristo ni la Kigiriki, na lilitungwa na Wagiriki baadaye, kutokea huko Antioki, Syria.
Mbali na kuwa jina la Kiebrania, na jina la mwanzo la dini hii hapo Yerusalemu, neno DEREKHI lina maana kubwa zaidi kidini kuliko neno UKIRISTO, au ‘Wafuasi wa Kristo’. Maana ya neno DEREKHI ni NJIA ya Mungu, Barabara ya Lami, iliyojengwa na Mungu mwenyewe ili sisi watoto wake tuipitie kuweza kufika kwenye hatma zetu, afya njema, mafanikio ya kidunia, na hatimaye uzima wa milele mbinguni. Kitabu kitakatifu cha Mikra (Biblia kwa Kigiriki) nacho kinaiita dini hii kuwa ni Njia ya Mungu au DEREKHI
Lakini Sauli akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, alimwendea kuhani mkuu, akataka ampe barua za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu (Mdo 9:1-2)
Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku, katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano. (Mdo 19:9)
Ona kwamba neno Njia linaanza na herufi kubwa katikati ya sentensi. Unaweza pia kusoma (Mdo 19:23), (Mdo 22:4), (Mdo 24:14), (Zab 67:1-2), (Zab 27:11), (Mit 22:6)
UDEREKHI wa Yerusalemu ulipitia misukosuko mingi kati ya Wayahudi wanaouunga mkono, na wanaoupinga. Katika mapingano hayo ya Wayahudi, Wagiriki ambao walikuwa wanaishi hapo Israel hata kabla ya Bwana Yesu kuzaliwa, walichukua hatamu za dini na kuihubiri dini nje ya Israel na baada ya muda, wakatafsiri vitabu vyote vya dini katika Kigiriki, na kwa hiyo wakaihubiri dini kwa Kigiriki na siyo kwa Kiyahudi, na wakatunga jina jipya la dini ambalo ni la Kigiriki, yaani Ukiristo. Jina hili halikuwa halali kwa sababu ni la Kigiriki, lakini pia linatoka katika maana halisi ya dini. Ukiristo wa Wazungu ulizaliwa na Ukiristo wa Wagiriki, na ndiyo maana unaendelea kutiumia Kigiriki katika dini mpaka leo.
DEREKHI AFRIKA inarekebisha kasoro hii kwa kurudi kwenye Kiebrania na Kiaramaiki, ambazo ndizo lugha za Wayahudi, Ukiristo (Kigiriki) unaitwa UDEREKHI, Yesu Kristo (Kigiriki) anaitwa ISHO HAMASHIACH, Biblia (Kigiriki) inaitwa MIKRA, Jehovah (Kigiriki) anaitwa YAHWEH, Sabato (Kigiriki) inaitwa SHABBAT, Kalvari (Kigiriki) inaitwa GOLGOTHA, nk
Maneno DEREKHI na KRISTO yote yanatumika kama majina ya kiume ya watu wa dini hii (kwa mfano Mcheza mpira maarufu wa Kireno, Christian Ronaldo) na hii haina tatizo lolote, lakini kwa sababu sasa tunajiengua kutoka katika Kigiriki, na tunarudi kwenye Kiebrania, basi tutakuwa tu na wanaume wanaoitwa DEREKHI lakini siyo CHRISTIAN.
Dini ya DEREKHI ilifika Ethiopia mwaka 330, na likaundwa dhehebu kongwe linaloitwa ETHIOPIAN ORTHODOX TEWAHEDO CHURCH. Dini ilikabidhiwa katika Ufalme ulioitwa Axum, ambayo ndiyo Ethiopia ya Kale inayoundwa na majimbo ya Tigray na Amhara. Watu hawa hawakuufundisha Uderekhi kwa Waafrika wengine mpaka walipofika Wareno pwani ya Afrika Magharibi mwaka 1450. Wareno walileta Kanisa Katoliki la Roma.
2) UDEREKHI WA DUNIA
Dini ya DEREKHI ilipoanza hapo Yerusalemu, ilipelekwa na mitume katika maeneo tofauti ya Mashariki ya Kati lakini ikawa inaendeshwa kwa ushirikiano. Yaani kulikuwa na dhehebu moja tu la dunia yote linaitwa Katoliki (Kigiriki) kikimaanisha dhehebu la watu wote. Kulikuwa na vituo vitano vya kidunia vinavyoongozwa na Maaskofu Wakuu lakini wanaoshilikiana na kuwa na mafundisho mamoja. Vituo hivi vilikuwepo Yerusalemu, Antioki (Syria), Alexandria (Misri), Constantinople (Uturuki) na Roma (Italia). Jinsi wakati ulivyokwenda, Maaskofu wa vituo hivi wakaanza kuhitilafiana na hatimaye wakagawanyika kuwa madhehebu tofauti mwaka 451, na tena mwaka 1054.
Sasa hivi UDEREKHI wa dunia unagawanywa katika makundi matatu makubwa kama ifuatavyo; –
- Uderekhi wa Magharibi (Kanisa la Roma, Makanisa ya Kiprotestanti, KIpentekosti)
- Uderekhi wa Mashariki (Greek Orthodox, Russian Orthodox, nk)
- Uderekhi wa Oriento (Syrian Orthodox, Ethiopian Orthodox, nk)
3) UDEREKHI WA MAGHARIBI
UDEREKHI wa Magharibi nao hugawanywa tena katika makundi makuu matatu, yaani; –
- Kanisa Katoliki la Roma
- Madhehebu ya Kiprotestanti ya Ulaya Magharibi (Lutheran, Anglican, Mennonite)
- Madhehebu 100+ ya Kipentekosti ya Kimarekani, na makanisa binafsi zaidi ya laki moja
UDEREKHI wa Magharibi ulianza na dhehebu moja la Roma, lakini mwaka 1530, Ujerumani, ikiongozwa na Padre Martin Luther, ikajitenga nalo na kuunda dhehebu linaloitwa kwa jina lake, Lutheran, na mwaka 1543, Uingereza nayo ikajitenga na Roma kwa kuunda dhehebu lake la Anglican. Madhehebu haya yaliitwa Protestant au Wapinzani wa dhehebu kuu la Roma. Mmeguko huu kutoka kwenye Kanisa la Roma ulishika kasi baada ya Wazungu kuanza kuhamia bara la Amerika, kuanzia mwaka 1600.
Uderekhi wa Magharibi ndio mkubwa zaidi duniani kwa wingi wa waamini, kwa sababu umechukua sehemu kubwa ya dunia. Unajumuisha Ulaya Magharibi yote, Amerika Kaskazini na Kusini, Afrika Kusini mwa Sahara yote, Australia, New Zealand, Philippines, Lebanon nk. Dhehebu la Roma ndilo dhehebu kubwa zaidi duniani likiwa na asilimia 50% ya Waderekhi wote duniani. Dhehebu hili hata hivyo limeporomoka katika eneo la Afrika Kusini mwa sahara. Asilimia ya dhehebu hili ya Waderekhi wote Afrika Kusini mwa Sahara imeshuka kutoka asilimia 90% mwaka 1920 hadi asilimia 40% mwaka 2020 kutokana na wimbi kubwa la madhehebu mengi mno ya Kipentekosti kutoka Marekani, pamoja na makanisa binafsi. Mwaka 2024, Afrika Kusini mwa Sahara ilikuwa na Madhehebu ya Derekhi zaidi ya 30 kutokea Marekani, na makanisa ya watu binafsi zaidi ya 30,000.
Makanisa binafsi ni zao la Uderekhi wa Marekani, unaoendeshwa kama biashara na siyo kama dini.
4) UDEREKHI WA MASHARIKI NA ORIENTO
Madhehebu ya DEREKHI ni mengi mno duniani, lakini madhehebu makubwa ya mashariki ni haya; –
- Greek Orthodox
- Syrian Orthodox
- Alexandria Coptic Orthodox
- Ethiopian Orthodox
- Russian Orthodox
Makanisa ya Mashariki na Oriental karibu yote hutumia neno Orthodox lakini yanatofautiana katika mafundisho. Madhehebu haya mengi yana makanisa yao nchi za magharibi pia, kwa ajili ya watu wa asili yao waliohamia huko Magharibi ambao ni wengi. Kwa jinsi hii, kuna makanisa ya Ethiopian Orthodox Tewahedo katika miji zaidi ya kumi huko Marekani. Kila dhehebu la Derekhi linabeba pia utamaduni wa nchi linakotoka, na ndiyo maana madhehebu yanafuata watu wao huko waliko.
5) DEREKHI AFRIKA
DEREKHI AFRIKA ni DEREKHI iliyoumanishwa na utamaduni mpana wa Mwafrika. Hili si jambo linaloeleweka sasa kwa Waafrika walio wengi, lakini litaeleweka huko twendako. Waafrika wa sasa hawaelewi mpaka leo kwamba dini ni sehemu kubwa sana ya utamaduni wa jamii fulani. Hii ndiyo kusema, basi, kwamba Uderekhi wa Magharibi uliojaa Afrika Kusini mwa Sahara unawakilisha ukoloni wa Utamaduni.
Mungu anawapokea watu wa tamaduni zote lakini ni juu yetu sisi Waafrika kuutetea na kuuheshimisha utamaduni wetu. Nahau ya Kiswahili inasema, “Mkataa kwao ni mtumwa.’ Ni lazima sisi Waafrika tuwe katika dini ya Kiyahudi iitwayo DEREKHI, lakini pia tuwe katika utamaduni wetu.
Wazungu waliileta dini hii hapa miaka 400 iliyopita na ilipaswa kuwa imekwisha kabidhiwa kwetu ili sisi tuiendeshe kutokana na mazingira yetu. Hili halijafanyika, na siyo tatizo la Wazungu; ni tatizo la Waafrika kukosa uwezo wa kujiongoza na kungangania utegemezi. Dini ni kitu rahisi, na ni kitu binafsi cha mtu. Kila mtu anajiongoza mwenyewe kutii amri za Mungu na hivyo kuwemo katika NJIA ya Mungu iliyotiwa lami iitwayo DEREKHI, au kujitungia njia zake za vichakani. Kwa hiyo dhehebu halina mchango mkubwa katika Uderekhi wa mtu. DEREKHI ni kile kitabu kitakatifu cha Mikra (Biblia), na siyo dhehebu.
6) UKUBWA WA DEREKHI
Kwa mujibu wa utafiti wa Kampuni kubwa ya utafiti ya Kimarekani iitwayo Pew Research, mwaka 2022, DEREKHI ndiyo dini kubwa zaidi duniani ikiwa na asilimia 31.2% ya binadamu wote, ikifuatiwa kwa karibu na Islam yenye asilimia 24.1%. Pew Research hata hivyo inasema, kwa kuangalia mwenendo wa asilimia hizi wa miaka 50 iliyyopita, asilimia ya DEREKHI inaendelea kushuka, kwa sababu kasi yake ya kuongeza waamini ni ndogo kuliko ongezeko la watu duniani. Uisilamu ndiyo dini inayokua kwa kasi kuliko ongezeko la watu na hivyo kuongeza asilimia yake kidunia. Hapa Afrika Kusini mwa Sahara, DEREKHI inaripotiwa kuwa na wafuasi 700 milioni, asilimia 68% ya Waafrika Weusi wote.
7) GHARAMA KUBWA YA KUENDESHA DEREKHI
UDEREKHI kila mahali unajiendesha kwa gharama kubwa sana kifedha ingawaje manufaa unayoleta kwa Mungu kwa maana ya asilimia ya watu wake wanaotembea katika NJIA ya Mungu ni machache sana. Moja ya sababu ya gharama kubwa za uendeshaji wa dini hii ni miundo mipana sana isiyoweza kuhalalishwa na majukumu ya dini. DEREKHI ya Wazungu inajiendesha kama serikali, ikiwa na utitiri wa watumishi, maofisi, nyumba za wafanyakazi, vyeo vikubwa, maghari ya watumishi nk. Haya yote ni ya kidunia tu, na hayajengi dini. Kwa miaka 1400, UDEREKHI wa Ulaya ulikuwa ni sehemu ya Serikali na kwa jinsi hii ulikuwa unagharimiwa na kodi siyo na sadaka za hiari.
Madhehebu ya Wazungu hapa Afrika yamekuwa hodari zaidi kutoa huduma za kijamii kama mashule na hospitali na siyo zile za kiroho ambazo ndizo wajibu wao.Ufundishaji na ufuatiliaji wa mambo ya kiroho umekuwa mdogo, na watumishi wanatumia muda mwingi kuhamisha waamini kutoka kwenye dhehebu hili kwenda lingine. DEREKHI pia ina watumishi wengi mno kwa kila waamini 1,000 kulinganisha na dini zingine zote duniani. Utumishi wa DEREKHI sasa umekuwa ajira siyo wito.
8) UKASISI WA WAAMINI
DEREKHI ya Wazungu inasimama kwenye Mapadre, Wachungaji, Maaskofu na Mapapa, lakini DEREKHI AFRIKA inaukataa muundo huu wa Kiaskofu na kuamua kurudi kwenye muundo uliotumika katika miaka ya Mwanzo ya DEREKHI kote Mashariki ya Kati ambao ulikuwa ni muundo wa Mabaraza ya Waamini. Mbele ya Mungu, waamini wote ni wa daraja moja kama inavyothibitishwa na neno la Mungu
Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkahihubiri injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa. Na ishara hizi zitaambatana nao waaminio;
Kwa jina langu watatoa pepo;
Watasema kwa lugha mpya;
Watashika nyoka;
Hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhulu kabisa;
Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata afya. (Mk 16:15-18)
Tunaona hapa kwamba Isho (Yesu kwa Kigiriki) hakutofautisha watumishi na waamini wa kawaida, bali aliwapa wote vipaji vilevile, na kinachoamua ni imani, siyo cheo cha utumishi.
Mungu akasema na tumfanye mtu, kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale Samaki wa baharini na ndege wa angani, na Wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu yan chi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; kwa mfano wa Mungu aliwaumba mwanamume na mwanamke aliwaumba. (Mwa 1:26-27)
Mungu ni roho, na kama aliwaumba watu kuwa kama yeye, ina maana binadamu pia ni roho, na mwili ni vazi tu walilovaa wawapo duniani. Hadhi hii ya kuwa roho, ni ya kila mtu, na inalingana na tamko la Isho, kwamba sote tuwe na nguvu za Roho juu yetu. Na huu ndiyo msingi wa UKASISI wa WAAMINI. Hii ndiyo kusema, Sakramenti za Utumishi, ni za kidunia, na hazina misingi katika Roho au katika maandiko. Kwa jinsi hii, UDEREKHI ni Udugu wa imani (Brotherhood), au Chama cha Ushirika wa Kidini (Spiritual Fraternity) kinachoundwa kusaidiana katika lengo kuu la sisi sote kutembea katika NJIA ya Mungu.
Hadhi hii ya Ukasisi wa kila Muamini, inaweka pia mkononi mwa kila muamini, wa jinsia yoyote, jukumu na dhamana ya UMISIONARI, wa kueneza dini hii, popote anapotokea kuwa, bila kutafuta idhini ya mtu mwingine yeyote. Kwa hiyo Wafanyabiashara, Wahandisi, Wakulima, Madaktari, Wanamichezo, na wengineo wa dhehebu hili ni MAKASISI na ni WAMISIONARI. Tunahitaji sote kujiandaa na kujipa ujasiri wa kufanya majukumu haya popote tutakapotokea kuwa.
Kwa mujibu wa tafiti za Wamarekani, DEREKHI ilikuwa na asilimia 68% ya Waafrika Weusi wote mwaka 2022 lakini DEREKHI AFRIKA inawatafuta Waafrika Weusi wote kujiunga nayo, na jukumu la kuwaleta Waafrika wote katika DEREKHI, kiuhalisia, ili watembee katika NJIA ya Mungu, na siyo tu wabatizwe, tunaliweka mabegani mwa kila muamini. NJIA iliyotiwa lami na Mungu mwenyewe ipo, na ni ya bure; hakuna sababu kwa Mwafrika yoyote kuendelea kupita vichakani kuliko na nyoka na kila aina ya dhahama. Katika DEREKHI AFRIKA tuna Mchungaji mmoja tu, Isho Hamashiach, katika Sinagogi zote, na halafu, tuna Shamashim (Wajakazi) wanaomsaidia Mchungaji. Kila muamini azungumze moja kwa moja na mchungaji wake.
Mimi ndiye mchungaji mwema, na walio wangu nawajua, na walio wangu wanijua mimi (Yn 10:14)
9) UTAWALA WA WAZEE WALIOCHAGULIWA
Utawala limekuwa jambo kubwa sana katika dini hii ya DEREKHI kuliko ilivyo kwa dini zingine zote duniani. Hii inatokana na historia ya dini hii kwamba ilikuwa pia ni serikali kwa zaidi ya miaka 1,000 huko Ulaya. Kidunia, DEREKHI ina miundo mitatu ya utawala kama ifuatavyo.
- EPISCOPAL; Utawala wa Kiaskofu na Mapapa
- CONGREGATIONS: Utawala wa Waamini wote kupitia mikutano mikuu
- ELDERS: Utawala wa Kamati za Wazee zilizochaguliwa na waamini
DEREKHI AFRIKA imeamua kuachana na mfumo wa utawala wa UDEREKHI wa Magharibi ambao ni wa Papa, Maaskofu na Mapadre/ Wachungaji, na badala yake kwenda kwenye utawala wa Kamati na Mabaraza ya Wazee (ELDERS) waliochaguliwa na waamini wote kwa miaka mitatu mitatu. Muundo huu wa kidemokrasia unaileta dini kwa waamini na kupunguza gharama za kuendesha dini. Huduma za kiroho zitatolewa na Shamashim (Wajakazi), na wote watakuwa na cheo kimoja tu hiki cha Shamashim (Kiebrania).
Tunaposoma maandiko, tunaona pia kwamba Sinagogi nyingi zilizoundwa na mitume wa mwanzo nje ya Israel ziliendeshwa kwa muundo huu wa kuwategemea wazee. (Mdo 11.30), (Mdo 14:23), (Efe 3:6-10), (1 Pet 2:9) (Efe 2:19-22), (1 Kor 12:12-27), (Mdo 15:2), (Mdo 20:17), (Tit 1:5), (Yak 1:5-14). Muundo huu pia unatupa nafasi kubwa zaidi ya kutekeleza falsafa ya Ukasisi wa Waamini wote.
10) DEREKHI YERUSALEMU
Dhehebu la kwanza lilianziahwa Yerusalemu na ndilo lilikuwa makao makuu ya dini. Baadaye dhehebu hili lilikufa kutokana na Wayahudi wengi kukataa kwamba Isho (Yesu kwa Kigiriki) hakuwa Ha-Mashiach (Kristo kwa Kigiriki). Pamoja na kukataliwa kwa DEREKHI na Wayahudi, DEREKHI bado ni dini ya Wayahudi, na bado Makao Makuu yake yapo mjini Yerusalemu. Maandiko yanasema hivi kuhusu Yerusalemu na kuhusu dini hii; –
Nyinyi Wasamaria mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi (Yn 4:22)
Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kiristo atateswa na kufufuka siku ya tatu na kwamba mataifa yote yatahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi kuanzia tangu Yerusalemu. (Lk 24:46-47)
Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mahusia ya Mungu. Ni nini basi ikiwa baadhi yao hawakuamini?, Je? Kutokuamini kwao kutaubatilisha uaminifu wa Mungu kwao? Hasha. (Rum 3:1-4)
Na mataifa mengi watakwenda na kusema; Njooni twende juu mlimani kwa Mwenyezi Mungu, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha NJIA zake, nasi tutakwenda katika mapito yake, kwa maana, katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu (Mik 4:2)
11) MIKRA TAKATIFU
Kitabu Kitakatifu cha Mungu kinachobeba Agano la Kale na Agano jipya kinaitwa Biblia kwa Kigiriki au Mikra kwa Kiebrania, na DEREKHI AFRIKA imekikataa Kigiriki, na inatumia Kiyahudi tu.
Mikra ni kitabu kikubwa sana, na ni kigumu kukielewa vizuri. Kwa hakika, hakuna mtu anayeweza kuilewa Mikra kwa akili yake , kwa kuisoma, au kwa kufundishwa kwenye Chuo cha Dhehebu. Uelewa sahihi unapatikana tu kwa Ufunuo wa Roho Mtakatifu, au neema ya Mungu mwenyewe. Ufunuo wa Roho haubadilishi maandiko, bali unatoa tafsiri sahihi ya NENO la Mungu. Duniani kumekuwa na upotoshaji mwingi wa dini hii unaotokana na tafsiri za neno za binadamu. Madhehebu makubwa na makongwe yametoa matamko ya kushangaza sana kuhusu dini hii ya DEREKHI.
Ni vizuri kuwa na Mikra nyumbani kwa kila muamini, na ni vizuri pia kujisomea Mikra, lakini ni lazima pia kuwasikiliza watu wachache wenye Ufunuo wa Roho juu ya kitabu hiki.
Lipo pia tatizo la Tafsiri ya kitabu hiki, ndiyo maana kila dhehebu kubwa lina Mikra yake, na unapozipitia Mikra za madhehebu mbalimbali, unaona kuna tofauti ndogo ndogo. Mikra ilitafsiriwa kutoka Kiyahudi kwenda Kigiriki, na baadaye Warumi wakatafsiri Kigiriki kwenda Kirumi, na baadaye Martin Luther akatafsiri Kirumi kwenda Kijerumani mwaka 1520, na baadaye Waingereza wakatafsiri Kirumi kwenda Kiingereza mwaka 1543. Kuanzia mwaka 1880, Wazungu walianza kazi kubwa ya Kutafsiri Mikra katika lugha nyingi sana za Kiafrika, kikiwemo Kiswahili. Neno hapa ni kwamba DEREKHI Afrika itaandika nayo Mikra yake kwa kufanya tafsiri mpya kutoka vitabu vya Kiyahudi
12) EMONAH
Neno la Kiebrania EMONAH lina maana ya imani na ni neno zito sana katika dini hii ya DEREKHI AFRIKA kwa sababu dini imesimama tu katika Emonah. Kuemona ni kujikabidhi kwa Mungu ili hatima yako hapa duniani, iamuliwe naye. Emonah ndiyo nguzo kuu lakini pia hakuna Emonah bila matendo. Ni lazima tutembee katika NJIA ya Mungu ili kuhesabika tunayo Emonah.
Basi imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.(Heb 11:1)
Ndugu zangu, yafaa nini mtu akisema anayo imani lakini hana matendo? Je hiyo imani yaweza kumuokoa? (Yak 2:14)
(Soma Ukurasa wetu wa EMONAH kwa elimu zaidi)
13) MUNGU
Dini ya DEREKHI inamilikiwa na Mungu aitwaye YHWH, au kwa urahisi, Yahweh. Wagiriki walitafsisi jina hili la Mungu kwenda kwenye Kigiriki na wakamwita Yehovah, lakini huku ni kutomheshimu Mungu. Jina lake lipo katika Kiyahudi na hairuhusiwi kulitafsiri. Mungu ni Mmoja tu, na dhana ya Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu ni upotofu wa kushangaza na kusikitisha kwa kupingana na Mikra. Mungu Baba ndiye pekee Mungu. Isho Hamashiach ni Mwana wa Mungu, lakini si Mungu, ni msaidizi wa Mungu aliyekasimiwa Madaraka na Mungu. Roho Mtakatifu ni mkono wa Mungu utendao kazi kwa niaba yake lakini si Mungu. Utukufu wa Mungu ni wa kipekee sana, na ni muhimu kulizingatia hili katika kila jambo, la kiroho, na la kidunia.
Isho Hamashiach (Yesu Kristo kwa Kigiriki) ndiye Mchungaji wetu, Kuhani Mkuu, Bwana na Mwokozi, asimamaye kati ya Mungu na Wanadamu. Isho pia ndiye njia ya kufika kwa Mungu, na mwombezi wetu mkuu kwa Mungu. Kila muamini ana ruhusa kuomba moja kwa moja kwa Mungu kwa jina la Isho, Bwana na Mwokozi. (Soma Ukurasa wetu wa DOCTRINE kwa elimu zaidi)
14) UAFRIKAJI WA DEREKHI
DEREKHI ni ya binadamu wote dunia nzima, lakini tunapotazama, tunaona kila dhehebu la DEREKHI, limebeba pia vipengele kadhaa vya utamaduni wa taifa linakotoka dhehebu. Wakati umefika sasa kwa Afrika nayo kuweka utamaduni wake katika DEREKHI. Utamaduni wa Afrika unamilikiwa na makabila zaidi ya 900, lakini yamo mambo mengi mno yanayofanana katika makabila mengi sana. DEREKHI Afrika ni ya Kiyahudi lakini itakuwa na vionjo kadhaa vya wazi vya Utamaduni wa Kiafrika.
Hatuna haja ya kuwa na DEREKHI ya kila kabila, au kila nchi ya mkoloni, kwa sababu tunataka kuunda dhehebu lenye nguvu, na ambalo litatoa mchango mkubwa sana katika kuunda ustaarabu wa Mwafrika (African Civilisation), ambao kwa hiyo hautaitwa Usta-Arabu, bali utaitwa Usta-Afrika. Watafiti wa Kizungu wanasema makabila 440 ya Afrika Kati, Mashariki na Kusini ni ya kibantu na tayari yana utamaduni na lugha zinazokaribiana, na DEREKHI AFRIKA itajenga juu ya msingi huo.
Baadhi ya Waafrika wanataka kuifanya DEREKHI kuwa sehemu ya siasa za Afrika kwa kuwa na dhehebu la kila nchi kama DEREKHI Zambia, Tanzania, Kenya, Ghana, Angola nk. Huu ni utoto kwa sababu sote tunaona kwamba madhehebu ya Ulaya Magharibi na Marekani yaliyofurika Afrika Kusini mwa Sahara, yapo kila nchi, Kwa hiyo sisi hatuna haja ya kuiga utoto wa Uingereza waliounda Church of England mwaka 1543. Lakini Church of England iliundwa kisiasa kutimiza matakwa ya Mfalme wa wakati huo, na sisi hatuendi huko. DEREKHI AFRIKA ni ya Afrika Kusini mwa Sahara yote na kila nchi itakuwa na tawi lake la dini hiyo hiyo. (Soma ukurasa wetu wa AFRICANISATION kwa elimu zaidi)
Waafrika hatuna haja ya kupitia kwa Wazungu kumfikia Mungu au Bwana Isho Hamashiach.
Na kondoo wengine ninao ambao si wa zizi hili, na hao nao imenipasa kuwaleta, na sauti yangu wataisikia, kisha kutakuwepo kundi moja na mchungaji mmoja.(Yn 10:16)
15) MADHEHEBU YA WAAFRIKA
DEREKHI AFRIKA inatambua kwamba hili siyo dhehebu la kwanza la Waafrika. Waafrika walianza kuunda madhehebu yao ya dini ya DEREKHI kuanzia miaka ya 1880 huko Kongo na Afrika Magharibi, na kufika, mwaka 2020, kulikuwa na madhehebu ya DEREKHI ya Waafrika zaidi ya 100. Madhehebu yanayozungumzwa hapa siyo Makanisa binafsi, ambayo yapo zaidi ya 30,000 sasa. Madhehebu binafsi yanaendeshwa na Waafrika lakini si ya Kiafrika, ni ya Kipentekosti, na yanahubiri Uderekhi wa Marekani. Hata yale Madhehebu Makuu ya Wazungu nayo yanaendeshwa na watu weusi lakini ni ya kigeni. Madhehebu ya Waafrika yanayozungumzwa hapa ni yale tu yaliyoanzia hapa Afrika, na mengi yake yanajumuisha UDEREKHI na Dini za jadi za makabila. Madhehebu haya ni potofu na ni madogo madogo sana.
DEREKHI AFRIKA ni Dhehebu pekee la Kiafrika, linalotokana na Ufunuo wa Roho, na utafiti mrefu sana wa maandiko, ndani na nje ya Mikra Takatifu. Linahubiri UDEREKHI halisi wa Yerusalemu, lakini limevaa utamaduni na jadi za Afrika, zisizokuwa za kiroho.
16) NYARAKA ZA DEREKHI AFRIKA
Ili kuonyesha kina kirefu ambacho DEREKHI AFRIKA inacho katika dini hii, ambacho ni kirefu kuliko hata kile cha madhehebu kongwe ya Wazungu, imetoa nyaraka tatu za kuiongoza katika kuwaendea Waderekhi wote milioni 700 katika nchi 42 za Afrika Kusini mwa Sahara. Nyeraka hizi ni.
- AFRICAN DEREKH; Unified and Africanised Christianity
Historia ya DEREKHI, Falsafa ya Dhehebu, Emonah, na Katiba, kurasa 150
2. D’VAR ELOHIM; Explication of God’s Revealed Word
Ufafanuzi wa Neno la Mungu, Uendeshaji wa Knesiya, kurasa 120
3. ORDER OF SHABBAT KHENES KADOSH
Mwongozo wa Ibada za Sabato/ Jumapili, kurasa 40
17) UPONYAJI NA UFUNGULIVU
DEREKHI ni dini inayosimama katika matumizi ya mara kwa mara ya nguvu za Mungu, katika KUPONYA, KUFUNGUA vifungo vya Uchawi, na KUTENDA MIUJIZA. Uponyaji na Ufungulivu vinatolewa na Roho Mtakatifu, na vinapatikana kwa jina la Isho Hamashiach (Yesu Kristo kwa Kigiriki)
Mtafuteni Mungu na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote (1 Nyk 16:11)
Lakini mtapokea nguvu akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu (Mdo 1:8a)
Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho, na za Nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
Tunakatazwa, kwa hiyo, tusihubiri DEREKHI kwa maneno tu, bali pia tudhihirishe, mara kwa mara, nguvu za Mungu, kama nyenzo kuu ya kujenga Emonah. Nguvu hizi zinadhihirishwa zaidi katika huduma ya Kuponya magonjwa na Kufungua.uchawi.
Huduma hii ya Ufungulivu ni ya thamani sana kwa Afrika Kusini mwa Sahara iliyogubikwa na uchawi na kulogana. Matumizi ya uchawi yameongezeka sana Afrika katika miaka 50 iliyopita pamoja na kuongezeka kwa utitiri wa madhehebu ya Kipentekosti ya Marekani. Yaonekana Waafrika walio wengi hawamwamini Mungu, na tuseme hawamjui. Ikitokea shida yoyote ndogo wanakimbilia kwa wachawi, waganga, waaguzi, wapiga ramli, matambiko, nk. Moyo wa kutu na moyo wa wivu umeendelea pia kupanuka ndani ya Afrika, hivi kwamba watu wengi bado wanajitaabisha kutafuta uchawi ili wawaloge, wawafunge, na kuwakomoa, ndugu zao, jirani zao, au washirika wao. Badala ya kufanya biashara kwa utafiti na kuyasoma masoko, bado asilimia kubwa sana ya Wafanyabiashara Weusi wanategemea uchawi, hirizi na mazindiko kufanya biashara zao. Lakini Wahindi, Wazungu na wageni wengine wasiotumia uchawi wowote bado wanawashinda wafanya biashara wa Kiafrika mara 100 zaidi. Walewale wanaojiita Waderekhi (Wakiristo) ndio pia wachawi, wavaa hirizi, wapiga ramli, waiba nyota za watu, nk.
Tunawaomba Waafrika waondoke kwenye maelfu ya Makanisa binafsi, na utitiri wa madhehebu ya Wazungu, na tuendeshe dini kitaasisi, na kimungu. Mtumishi asiyetaka kufanya kazi kitaasisi anaikana imani, na apumzike. Waafrika waache mihemuko ya kuwatafuta wahubiri fulani ili kusaidiwa, kwa sababu anayeponya na kufungua ni Mungu mwenyewe, naye anafanya hivi tu kama tutalitumia jina la Isho Hamashiach, Bwana, Mwokozi na Mchungaji wetu. Emonah katika Mungu na katika Isho, na ujasiri wa kuwaendea, vina nguvu zaidi kuliko upako wa mtumishi. Tunasema tena, kila Mderekhi ni Roho, ni Kasisi, na anayo nguvu, na ruhusa, ya kujiponya na kujifungua yeye mwenyewe hapo alipo kwa jina la Isho. Ni maswala ya kuelimishana, lakini pia kujenga uaminifu wa muda mrefu kwa Mungu. Tusiiache NJIA na kujipitisha vichakani kwa madai ya kutafuta oponyaji au mafanikio. (Soma Ukurasa wetu wa DELIVERANCE kwa elimu zaidi)
18) SINAGOGI
Nyumba za ibada za DEREKHI AFRIKA zitaitwa Sinagogi kwa sababu Bwana Mkubwa Isho Hamashiach mwenyewe alisali katika majengo yaliyoitwa Sinagogi, na Wayahudi bado wanasali katika majengo yanayoitwa Sinagogi. Sinagogi huitwa pia Beit Knesset.
DEREKHI AFRIKA itazingatia pia itifaki ya kale ya Sinagogi ikiwa ni pamoja na kuingia bila viatu, kukaa chini sakafuni, wanawake kuvaa vitambaa kufunika vichwa na shingo, na kuwa na utenganisho kamili kati ya wanaume na wanawake. Ni lazima wanawake wavae nguo zizizobana mwili, za mikono mirefu na ndefu mpaka kwenye viwiko vya miguu yao ili kuingia Sinagogi
Katika Sinagogi, Shamashim watakaa wakitazama mbele na watasimama kwenda mbele kuhudumu na kurudi kwenye nafasi zao. Ni wanaume na wavulana pekee wanaoweza kuhudumu Sinagogi, au kwingineko. Watumishi wa Sinagogi wataitwa Shamashim (Mjakazi) na watapitia mafunzo rasmi, kuidhinishwa na kuratibiwa katika utumishi wao.
19) MFUNGO WA MWAKA
DEREKHI AFRIKA inarejesha jadi ya kidini ya DEREKHI ya Mfungo Mkuu wa Mwaka wa siku 40 unaoishia Kifo cha Bwana Isho msalabani. Mfungo huu utahusisha kufunga chakula masaa 14 kuanzia saa 11 alfajiri, na kufanya matendo mengine ya kujishusha na kujidhili, ili kutubu dhambi.
20) SALAMU ZA DEREKHI AFRIKA
Katika shughuli za dini, na katika maeneo ya Sinagogi, Waafrika tutasalimiana kwa moja ya salamu hizi, kwa Kiebrania au kwa tafsiri ya lugha za makabila yetu.
KAVOD LELOHIM; (Atukuzwe Mungu Mkuu)
LEHOL LAHM (Tangu Milele, Hata Milele)
HALLEL HAMASHIACH; (Asifiwe Isho Mwokozi)
AMEN (Ameni)
SHALOM ALEKHEM (Amani ya Mungu iwe nawe)
ALEKHEM SHALOM (Iwe nawe pia)
21) MALENGO MAKUU
Kwa muhtasari DEREKHI AFRIKA imeamukia mambo yafuatayo; –
- Kuondoa mmeguko mkubwa sana wa dini ya DEREKHI usio na tija kwa Mungu wala kwa wanadamu ndani ya Afrika Kusini mwa Sahara. Mambo ya kumeguka meguka kwa dini yamo tu katika UDEREKHI wa Magharibi, na tuwaachie wao.
- Kukomesha kero za Waamini za kutafuta kusali kwenye makanisa ya madhehebu yao, na hivyo kusababisha baadhi ya waamini kusafiri kilomita 10 au zaidi kila jumapili kulifikia kanisa lao, wakati Uderekhi ni uleule.
- Utumishi ndani ya dini ya DEREKHI unahitaji usimamizi ili watumishi wasidhalilishe dini kwa ushetani wao binafsi. Usimamizi unapatikana tu ndani ya taasisi kubwa kama DEREKHI AFRIKA. Tunaziomba Serikali zote za Afrika zifute kwa sheria, makanisa binafsi ya DEREKHI.
22) KARIBU
- Karibu katika kuzaliwa upya kwa dini ya Mungu Mkuu, DEREKHI, hapa Afrika
- Karibu DEREKHI AFRIKA, chipukizi la DEREKHI Yerusalemu
Tembelea ukurasa wetu wa CONTACTS, na uwasiliane nasi, ili uwe sehemu ya kazi hii kubwa ya Mungu iliyo mbele yetu. DEREKHI AFRIKA haimilikiwi na mtu au watu, ni ya Mungu mwenyewe, na sote tuna haki na wajibu wa kushiriki, kama Waemona na Makasisi.
SHALOM ALEKHEM
DEREKHI AFRIKA
Juni 2025
Silvanus Mutagaywa Ngemera
Shamashim (Mjakazi) wa Kwanza
Tovuti: www.africanderekh.org
B-pepe: derekh@africanderekh.org
africanorthoderekh@gmail.com